Mtindo bora wa maisha ni kuishi kwa kuzingatia kanuni za afya na kwamba, mtindo bora wa maisha unahusisha kuzingatia ulaji bora, kufanya mazoezi ya mwili, kuepuka matumizi ya pombe, kuepuka matumizi ya sigara na bidhaa zinazotokana na tumbaku ikiwamo dawa za kulevya pamoja na kuepuka msongo wa mawazo.

Mojawapo ya faida ya mtindo bora wa maisha kwa afya ni kuzuia kupata maradhi hasa yanayotokana na mtindo wa maisha usiofaa na kwamba, ulaji bora kwa kufuata mtindo bora wa maisha utakuepusha na shinikizo kubwa la damu, ugonjwa wa moyo, kisukari pamoja na saratani mbalimbali.

Njia bora ya ulaji unaofaa kwa afya

Daktari bingwa wa afya ya jamii na familia kutoka Chama cha Afya ya Jamii (TPHA) Ali Mzige, anasema moja ya njia bora za ulaji unaofaa ni kula mlo kamili ambao una mchanganyiko wa aina mbalimbali za vyakula.

“Mlo huu hukuwezesha kupata virutubishi muhimu vya kukidhi mahitaji ya mwili, lakini mlaji anatakiwa kuwa makini na mwangalifu asile chakula chochote kwa wingi kupindukia na anatakiwa kubadilishana aina za vyakula katika kila mlo”, anasema Dk Mzige.

Anasema vyakula hivyo husaidia mwili kujikinga na maradhi mbalimbali pamoja na kutupatia makapi mlo ambao humfanya mtu ajisikie kushiba na kupunguza uwezekano wa mtu kuwa na uzito au unene uliozidi.

Anasema uzito au unene uliopitiliza huongeza hatari ya kupata maradhi kama shinikizo kubwa la damu, kisukari, maradhi ya moyo na baadhi ya saratani.

Chagua asusa zenye virutubishi muhimu

Mtalaam huyo anasema ni vyema mlaji akachagua asusa zenye virutubisho muhimu, hivyo ni lazima mtu awe makini katika kuchagua asusa zenye virutubishi vingi na muhimu kama matunda, maziwa, sharubati ya matunda (juisi halisi), karanga, vyakula vilivyochemshwa, vyakula vilivyookwa au kuchomwa kama ndizi, mihogo, mahindi na viazi.

Asusa ni chakula kinachoweza kuliwa kati ya mlo mmoja na mwingine.

“Epuka asusa zenye mafuta mengi, chumvi nyingi au sukari nyingi kwa sababu huweza kusababisha ongezeko kubwa la uzito, huweza pia kusababisha kupata kisukari, shinikizo la damu au maradhi ya moyo” anasema.

Neema Joshua ni mtaalam wa masuala ya lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) anafafanua kuwa ulaji unaofaa ni kuongeza kiasi cha makapimlo ambayo yatasaidia katika mfumo wa chakula lakini pia huchangia katika kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya saratani, matatizo ya moyo na ugonjwa wa kisukari.

“Kupitia makapi-mlo unayokula unaweza kuongeza kiasi cha makapi-mlo kwa kula matunda badala ya sharubati (juisi), kupika mboga kwa muda mfupi, kutumia unga wa nafaka ambazo hazijakobolewa na kula vyakula vya jamii ya kunde mara kwa mara”, anasema Joshua.

Madhara ya mafuta mengi

Licha ya kuwa mafuta ni muhimu katika mwili wa binadamu, wataalam wanasisitiza mafuta hayo yanahitajika mwilini kwa kiasi kidogo.

Mafuta yanapoliwa kwa kiasi kikubwa yanaweza kusababisha madhara mwilini kama kuongeza uzito, kuongeza uwezekano wa kupata maradhi ya moyo, kisukari pamoja na shinikizo la damu.

“Kutokana na hali hiyo, mtu anaweza kupunguza kiasi cha mafuta kwa kubadili njia za mapishi kama kuoka, kuchemsha, kuchoma badala ya kukaanga au kuchagua samaki au nyama isiyokuwa na mafuta pamoja na kuepuka asusa zenye mafuta mengi Dk Mzige.

Sukari nyingi

Dk Mzige anafafanua kuwa njia hii watu wengi wa rika mbalimbali hushindwa kujizuia na kutumia vitu vitamu kama biskuti, chocolate, keki, sharubati bandia, pipi, soda na hata ice cream bila kujua madhara yake.

Anasema licha ya sukari kuongeza nishati mwilini, huongeza uzito ambao huweza kusababisha mtu kupata maradhi mbalimbali ikiwamo kisukari, lakini huchangia kuleta madhara kwenye meno.
Matumizi ya sukari nyingi unaweza pia kuipunguza kwa kunywa vinywaji visivyokuwa na sukari kama sharubati ya matunda halisi na hivyo kuepuka vyakula vyenye sukari.

Chumvi nyingi

Hata hivyo, mlaji wa vyakula vyenye chumvi nyingi  huchangia kuongeza uwezekano wa kupata shinikizo kubwa la damu, hivyo kukabiliana na hali hiyo, jamii inashauriwa kula vyakula ambavyo havijasindikwa kwa chumvi nyingi pamoja na kupunguza kiwango cha chumvi wakati wa kupika na kuwa na utamaduni wa kutoongeza chumvi ya ziada iliyopo mezani.

Wataalam wa lishe wanaeleza kuwa maji yana umuhimu mkubwa katika lishe na afya ya binadamu na mchakato wote wa lishe hauwezi kufanya vizuri bila maji.

Watu wanashauriwa kunywa maji angalau lita mbili kwa siku kwa sababu maji ni muhimu